Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa Goma

Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa Goma

Ladislaus Ntangazwa ambaye ni mmoja wa watuhumiwa Tisa wanaosakwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 amekamatwa usiku wa kuamkia Jumatano huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Tangazo la kukamatwa kwake limetolewa na mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Rwanda, ICTR Hassan Bubacar Jallow, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani.

(Sauti ya Jallow)

“Kwamba usiku wa kuamkia leo, mmoja wao alikamatwa na ni Ladslaus Ntangazwa, meya wa zamani wa eneo la Nyakizu huko Butare. Alikamatwa na sasa anashikiliwa. Alishtakiwa kwa makosa ya mauaji ya kimbari ya watutsi na uhalifu dhidi ya binadamu kwenye jamii hiyo, na maagizo aliyotoa ya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake wa kitutsi na uchochezi. Kesi yake imehamishiwa Rwanda ili iweze kusikilizwa. Hivyo taratibu zinafanyika aweze kuhamishwa kutoka Goma hadi Rwanda ili kesi isikilizwe kwa mujibu wa mfumo uliochukua majukumu ya ICTR.”

 Bwana Jallow alikuwa New York ambako wamewasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ripoti ya mwisho ya utendaji wa mahakama hiyo inapofikia ukingoni mwaka huu.

Amesema jukumu la kusaka na kufungulia mashtaka watoro wengine wanane ni la mfumo wa mahakama za uhalifu wa kimataifa, MICT, unaochukua majukumu ya ICTR na kwamba..

(Sauti ya Jallow)

 "Msako dhidi ya watoro wengine inapaswa kuendelea licha ya ICTR kuhitimisha majukumu yake. Halikadhalika naamini pia ufunguaji wa mashtaka dhidi ya watuhumiwa wengine zaidi ya 100 wanaoishi nchi nyingine unapaswa kufanya na nchi ambako wamesaka hifadhi au wanaweza kukamatwa na kupelekwa Rwanda. Na mwishoni tuna changamoto ya kuwapatia makazi mapya ya kuhamia watu walioachiliwa na sasa wako Arusha ili wapate makazi na kuishi huru.”

Wakati huo huo, Bwana Jallow amesema tarehe 14 wiki ijayo, ICTR itahitimisha kazi zake kwa kutoa hukumu ya kesi dhidi ya kesi ya Nyimaramasuhuko na wenzake inayohusisha watu Sita ikijulikana zaidi kama rufani ya Butare.