Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya haki za binadamu Ukraine bado ni ya mashaka:UM

Hali ya haki za binadamu Ukraine bado ni ya mashaka:UM

Ripoti ya Umoja wa mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Ukraine iliyotolewa leo mjini Geneva inasema mpango maalumu wa usitishaji mapigano mashariki mwa nchi hiyo umepunguza kwa kiasi kikubwa ukatili hasa katika mwezi wa Septemba na Oktoba.

Gianni Magazzeni ni mkuu wa haki za binadamu kanda ya Ulaya na Asia ya Kati.

(SAUTI YA GIANNI MAGAZZEIN)

"Kikubwa kipya kilichobainika ni kupungua kwa vifo vya raia na mauaji mengine kwa sababu ya kupungua kwa mapigano baina ya operesheni za vikosi vya serikali ya Ukraine na makundi yenye silaha. Hivyo kumekuwepo usitishwaji wa mapigano ambao umedumu”

Hata hivyo ripoti inasema vita vya silaha vinaendelea kuathiri maisha ya watu na haki za binadamu, inatoa ushahidi wa ukiukaji wa haki za binadamu na uhuru wa watu vikiwemo vitendo vya utesaji, kutoweka kwa watu , uhuru wao wa kutembea na kukiukwa kwa haki zingine. Imeongeza kuwa tangu katikati ya mwezi Aprili mwaka 2015 hadi Novemba 15 machafuko yamekatili maisha ya watu 9098 na kujeruhi wengine 20,732 nchini Ukraine.