Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji dhidi ya Malaria waleta nafuu kubwa:WHO

Uwekezaji dhidi ya Malaria waleta nafuu kubwa:WHO

Uwekezaji dhidi ya Malaria waokoa zaidi ya vifo Milioni Sita katika miaka 15 iliyopita.

Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO katika ripoti yake kuhusu Malaria iliyotolewa leo ikiangazia mafanikio hayo kutokana na malengo ya maendeleo ya milenia na mambo yaliyosalia kutekelezwa hadi mwaka 2030.

Mathalani ripoti inasema zaidi ya asilimia 50 ya nchi 106 zilizokuwa na Malaria mwaka 2000, zimepunguza visa vipya kwa angalau asilimia 75 mwaka huu.

Huduma za kinga dhidi ya Malaria kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la sahara, ikiwemo matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu,  zimeelezwa kuokoa zaidi ya dola Milioni 900 katika kipindi hicho kutokana na kutokuwepo wagonjwa.

Dkt Pedro L Alonso ni mkurugenzi wa mpango wa kimataifa wa Malaria kwenye WHO.

"Kuna maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka 15 juu ya visa vilivyoepukwa, maisha yaliyookolewa, karibu vifo Milioni sita viliepukwa, na faida za kiuchumi zitokanazo na hali hiyo. Lakini kila mara tunatambua kazi iliyosalia na visa vipya Milioni 214 ambavyo vimekuwepo mwaka huu pekee, vifo 438, 000 mwaka huu kati ya watu Bilioni Tatu nukta Mbili waliosalia hatarini kupata Malaria kwenye maeneo yaliyo hatarini zaidi.

Ili kutokomeza Malaria katika nchi 35 zilizosalia, WHO inataka uwekezaji wa dola kutoka karibu bilioni Tatu kila mwaka hadi dola Bilioni tisa kila mwaka ifikapo mwaka 2030.