Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna haja ya kulinda haki za kisiasa na kiraia DRC kuelekea uchaguzi:UM

Kuna haja ya kulinda haki za kisiasa na kiraia DRC kuelekea uchaguzi:UM

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Jumanne imetanabaisha hofu ya ukandamizaji dhidi ya upinzani, vyombo vya habari na asasi za kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC ) tangu mwanzo wa mwaka na inasisitiza haja ya kuhakikisha haki za kisiasa na kiraia kabla ya chaguzi muhimu.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(UNJHRO) imeorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu unaohusiana na mchakato wa uchaguzi kati ya Januari mosi na septemba 30 mwaka 2015, ikiwemo vitendo vya mauaji, vitisho vya kuuawa, kukamatwa na kuwekwa kizuizini, matumizi ya nguvu na vikosi vya usalama, na vikwazo wa haki ya uhuru wa kujieleza na mkutano wa amani.

Ripoti hiyo imeonya kuwa vitendo hivyo ya kukandamiza uhuru wa kujieleza na ukiukaji wa usalama wa wale wanaopinga serikali vinashiria kuzorota kwa fursa ya demokrasia na uwezekano wa kuathiri uaminifu wa mchakato wa uchaguzi.

Kwa ujumla rripoti hiyo imeorodhesha matukio 143 ya ukiukaji wa haki za binadamu unaoambatana na mchakato wa uchaguzi na ukiukaji mkubwa ulifanyika katika maeneo ambayo vyana vya upinzani na jumuiya za kiraia vinaushawishi mkubwa ikiwemo majimbo ya Kinshasa, Kivu ya Kaskazini na Kusini na Kasai Mashariki.