COP21 yaingia wiki ya pili, Ban ataka ahadi ziingie kwenye vitendo
Mkutano wa 21 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP21 umeingia wiki ya pili huko Paris, Ufaransa kwa kuanza kwa vikao vya ngazi ya juu.
Akifungua kikao cha leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema wakati umewadia sasa wa kubadili kuwa vitendo ahadi alizopatiwa na viongozi wiki iliyopita ya kudhamiria mkataba thabiti wa mabadiliko ya tabianchi kutoka Paris.
Amesema viongozi walimhakikishia kuwa watafanya kila kitu kuondoa vikwazo vya kufikia mkataba waa aina hiyo na sasa ni kazi ya watendaji na wataalamu kutafsiri ahadi hizo za kihistoria kuwa mkataba wenye vitendo, sahihi na sawia kwa wakazi wote wa dunia.
Baada ya ufunguzi huo, Katibu Mkuu alizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa..
(Sauti ya Ban)
“Tumebakiza siku za mashauriano zisizozidi nne. Masuala magumu yamesalia, na fursa kama hii ya kisiasa inaweza isipatikane tena. Nawasihi mawaziri na wataalamu walioko hapa kutopoteza fursa hii. Nina uhakika kuwa Paris inaweza kuwa fursa ya pekee ya kuelekea mustakhbali endelevu, wa afya na ustawi kwa wote.”