Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa uchaguzi Comoro, UM na wadau wapongeza ujumbe wa Kikwete

Mchakato wa uchaguzi Comoro, UM na wadau wapongeza ujumbe wa Kikwete

Umoja wa mataifa, muungano wa Afrika, muungano wa Ulaya na shirika la kimataifa la La Francophonie, wanafuatilia kwa karibu hali inayoendelea visiwani Comoro wakisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa magavana na rais ufanyike kama ulivyopangwa mwakani.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa hii leo imesema chaguzi hizo zimepangwa kufanyika mwezi Februari na Aprili mwakani na kwamba kufanyika kwake kutaimarisha maendeleo ambayo Comoro imepata kwa muongo mmoja uliopita baada ya mzozo wa kisiasa.

Taasisi hizo zimetambua kuwa tayari usajili wa wagombea umeanza tarehe leo tarehe Sita Disemba na wamepongeza ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini humo ulioongozwa na Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete tarehe 30 mwezi uliopita.

Kwa mantiki hiyo, taasisi hizo zimetaka wadau wa kisiasa kujiepusha kufanya vitendo vyovyote vinayoweza kupeleka mrama mchakato wa kisiasa na badala yake washirikiane kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa huru na haki kwa mujibu wa katiba ya nchi.