Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu nchi za Afrika kwa kupaza sauti moja COP21

Ban asifu nchi za Afrika kwa kupaza sauti moja COP21

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesifu hatua ya nchi 54 za Afrika kuzungumza kwa sauti moja kwenye majadiliano yanayoendelea kwa lengo la kuibuka na mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa.

Amesema hayo alipozungumza kwenye kikao cha mawaziri wa mazingira wa Afrika siku ya Jumapili akisema mwelekeo wa majadiliano unatia moyo lakini anatambua kuwa bado kuna masuala manne ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na hivyo Umoja ni nguvu.

Ametaja masuala hayo kuwa ni hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi, utofauti katika kugharimia hasara zitokanazo na madhara ya mabadiliko hayo, ari ya pamoja ya kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto mbili katika kipimo cha selsiyasi na nne ni fedha.

Ban amesema hakuna kurudi nyuma, lazima kusongesha mashauriano ili kuhakikisha mkataba unaopitishwa unakuwa na vigezo hivyo vinne kwa kuwa shughuli za kiuchumi za Afrika zinaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema nchi zilizoendelea zinapaswa kutambua kuwa kuwekeza Afrika ni mbinu ya kuweza kufanikisha ari ya kila mmoja na hatimaye kufanikisha makubaliano ya Paris.