Skip to main content

COP21,Ban atangaza hatua kwa mwaka 2016

COP21,Ban atangaza hatua kwa mwaka 2016

Mashirika mbali mbali mwakani yataunda ubia wa kusongesha kasi ya harakati za kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi kufuatia hatua zitakazochukuliwa kwenye mkutano wa mabadiliko ya nchi unaoendelea Paris, Ufaransa, COP21.

Hatua hiyo imetangazwa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipokuwa akizungumza ikiwa ni siku ya Sita ya COP21 iliyopatiwa jina la siku ya hatua au Action Day.

Ban amesema ametiwa moyo sana kwa kuungwa mkono na wigo mkubwa zaidi wa ubia wa mashirika na taasisi za wasomi kwa lengo la kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi ili kuibuka na fursa mpya.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na mkutano utakaondaliwa kwa ushirika na chuo kikuu cha Maryland tarehe Tano hadi Sita mwezi Mei mwakani huko Washington, DC ukileta pamoja viongozi wa serikali, majiji, vitongoji na wafanyabiashara.

(Sauti ya Ban)

“Haya ni maeneo ambayo yatasaidia kuleta tofauti kubwa wakati tunafanya kazi kutekeleza matokeo ya mkutano huu wa mabadiliko ya tabianchi hapa Paris. Tunahitaji kupanua haraka hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kila ngazi, kuanzia kitaifa hadi kimataifa.

Katibu Mtendaji wa kamati ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC Christiana Figueres akasema baada ya kutangazwa hatua hizo sasa ni wakati wa kubadilika kutoka siku ya kutangaza hatua hadi dunia inayochukua hatua akisema..

(Sauti ya Christiana)

"Ina maana kuanza kutekeleza mipango hii ambayo ni mizuri na imeangaziwa wiki nzima na hata leo.Mipango hii haihitaji kuwa iliyojadiliwa pekee bali ya kutumika na tunahitaji kufanya hivyo haraka sana ."