Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo si kuhusu hali joto, ni kuepukana na hewa ya ukaa: COP21

Mazungumzo si kuhusu hali joto, ni kuepukana na hewa ya ukaa: COP21

Waziri wa mambo ya nje wa ufaransa Laurent Fabius  amesema mazungumzo yanayoendelea kwenye mkutano wa 21 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP21 yanapaswa kusonga hatua zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Paris, Bwana Fabius amesema anatumai kwamba mapendekezo ya makubaliano yanayotarajiwa kuwasilishwa jumamosi hii yataonyesha hatua zingine, akisisitiza kwamba nchi zinapaswa kulegeza misimamo yao na kusaka mwafaka.

Kwa upande wake Katibu mtendaji wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya mkataba kuhusu makubaliano ya tabianchi, UNFCCC, Christiana Figueres amesema kwamba mazungumzo kuhusu kiwango cha hali joto ambacho kinapaswa kudhibitiwa kati ya nyuzijoto 1.5 na nyuzijoto 2 za Selisiasi hayatazuia mchakato wa kupata makubaliano kwa kuwa,

(Sauti ya Bi Figueres)

"Ni lazima kuepukana na hewa ya ukaa haraka, na kwenye sekta zote za uchumi. Ni hayo tunayojadili  tukizungumzia nyuzi 1.5 au 2. Mazungumzo si kuhusu hali joto, hiyo ni makadirio. Mazungumzo ni kuhusu kuepukana na hewa ya ukaa kwenye uchumi."