Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutumie udongo kwa njia endelevu: Ban

Tutumie udongo kwa njia endelevu: Ban

Kasi ya kupungua kwa rutuba ya udongo inaongeze na kuna umuhimu wa kubadili mwelekeo huo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wake kuelekea siku ya udongo duniani tarehe Tano mwezi huu wa Disemba.

Ban amesema udongo ni msingi wa mifumo ya vyakula na hivyo taarifa kwamba asilimia 33 ya udongo ulioko duniani umepungua rutuba ni za kushtusha.

Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kupitia matumizi endelevu ya udongo.

Wakati  Katibu Mkuu akitoa wito huo, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO katika ripoti yake kuhusu hali ya udongo duniani, limesema bado kuna fursa ya kubadili mwelekeo.

Fursa hizo ni pamoja na nchi kukubali kubadili mbinu za matumizi ya udongo wakati huu ambapo imeelezwa kuwa matumizi ya udongo duniani yataongezeka kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2050 kutokana na ongezeko la mahitaji ya chakula yachochewayo na ongezeko la idadi ya watu.

Siku ya kimataifa ya udongo inapoadhimishwa kesho, FAO imehitimisha mwaka wa kimataifa wa udongo, 2015 kwa kufanya tukio maalum kwenye makao makuu ya shirika hilo  huko Roma, Italia.