Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi mpya wa WFP kusaidia watoto na wakulima CAR

Mradi mpya wa WFP kusaidia watoto na wakulima CAR

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Shirika la Kimataifa la Mpango wa Chakula WFP limetangaza kupanua mradi wake mpya uitwao, Nunua kwa ajili ya Mabadiliko,  au kwa kiingereza Purchase for Progress, ili kufikisha msaada wa mlo wa shuleni kwa watoto 80,000.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WFP imeeleza kwamba mradi huo unalenga pia kuinua kipato cha wakulima wadogo wadogo 12,000 kwa kuboresha utaalam wao wa kulima mpunga na maharage, kuongeza mavuno yao na kuwawezesha kuuza sokoni mazao ya ziada.

Kupitia ufadhili wa Marekani, Ujerumani na Japan, WFP inalenga kununua zaidi ya tani 400 za mchele na maharage kwa ajili ya kulisha watoto shuleni.

Mkuu wa WFP nchini CAR, Bienvenu Djossa amesema mradi huo mpya hunufaisha wakulima wanaopata fursa mpya za kiuchumi na watoto pia ambao wanawezeshwa kusoma shuleni kupitia milo hiyo.

WFP imekumbusha kwamba watu milioni 1.8 wanakadiriwa kuhitaji usaidizi wa kibinadamu nchini CAR.