Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twatumai Rais Kagame atang’atuka 2017: Balozi Power

Twatumai Rais Kagame atang’atuka 2017: Balozi Power

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Samantha Power amezungumza na waandishi wa habari katika wadhifa wake wa Urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Disemba na kuelezea mipango yao ya kazi ikiwemo suala la Burundi.

Katika mkutano huo Balozi Power aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu mpango wa Rais Paul Kagame wa Rwanda kuongeza muda wa uongozi ambapo Balozi Power amesema

(Sauti ya Balozi Power)

“Rais Kagame ana fursa ya kuonyesha mfano kwenye ukanda ambao viongozi wanaonekana kushawishika sana  kujiona kuwa wao ni muhimu zaidi kwa nchi zao na bila wao haiwezekani. Tumeona mfano wa Rais Jakaya Kikwete akionyesha mfano dhahiri kwa kukabidhi madaraka kwa amani. Tunatarajia kwa dhati kuwa Rais Kagame atatimiza ahadi alizozitoa zamani, ili kuruhusu kizazi kipya cha viongozi kuja mbele na kusaidia kuongoza Rwanda iliyotoka mbali sana na kujikwamua katika nyanja mbali mbali, na hivyo kusonga hatua nyingine.  Kwa hiyo tunategemea Rais Kagame ataachia madaraka mwisho wa muhula wake mwaka 2017;”

Kuhusu Burundi amesema Baraza linafikiria kufanya ziara nchini humo, na kwamba linaanda mpango wa dharura ili kuchukua hatua hali ikizidi kuwa mbaya, lakini hata hivyo amesema hali ya Burundi haijalingana na ile ya Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari.