Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Milioni 40 zahitajika kukwamua afya za wayemen: WHO

Dola Milioni 40 zahitajika kukwamua afya za wayemen: WHO

Kadri mzozo nchini Yemen unavyozidi kushika kasi kila uchao, afya za wananchi nazo zinazidi kudhoofika huku watu Milioni 12 nukta Tano wakihitaji huduma hiyo muhimu.

Shirika la afya duniani, WHO limesema hii leo kuwa licha ya ukosefu wa usalama wadau wa afya wanahaha kutoa usaidizi lakini kikwazo sasa ni ufadhili kwani ukata unakwamisha operesheni zao.

Mathalani, WHO imesema ofisi zake huko Sana’a na Aden, zimekuwa ndio nguzo ya utoaji wa huduma za afya nchini Yemen na mwaka huu pekee zimesambaza tani 300 za dawa na kupatia vituo 71 vya afya siyo tu vifaa tiba bali pia mafuta ambayo uhaba wake umekwamisha kwa kiasi kikubwa operesheni za usaidizi.

Kwa mantiki hiyo WHO imesema inahitaji dola Milioni 46 kando ya dola Milioni 83 za ombi la dharura la usaidizi kwa Yemen, ikisema kuwa kiasi hicho ni kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya.