Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP21, Afrika kunufaika na uimarishaji mifumo ya tahadhari ya hali ya hewa

COP21, Afrika kunufaika na uimarishaji mifumo ya tahadhari ya hali ya hewa

Mpango wa kutoa onyo mapema kuhusu mabadiliko ya tabianchi, CREWS umezinduliwa leo huko Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa COP21 kama moja ya mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Tayari serikali za Australia, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Luxembourg zimekubali kupatia mpango huo zaidi ya dola Milioni 80 kwa ajili ya kuwezesha nchi 80 kuboresha mifumo yao ya tahadhari ya hali ya hewa, CREWS.

Nchi nufaika ni zile za Afrika na za visiwa vidogo ambazo zimekuwa wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi huku mifumo yao ya utambuzi na utoaji taarifa ikiwa ni dhaifu.

Michel Jarraud ambaye ni Katibu Mtendaji wa shirika la hali ya hewa duniani, moja ya waungaji mkono wa mpango huo amesema mifumo ya aina hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa madhara yatokanayo na vimbunga, moto wa misituni, tsunami na mawimbi joto baharini.

Mfumo huo ulipendekezwa na Ufaransa huko Japan na sasa unaungwa mkono na shirika la hali ya hewa duniani, WMO, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga, UNISDR na benki ya dunia.