Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria za vita zaendelea kuvunjwa Syria

Sheria za vita zaendelea kuvunjwa Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema kwamba kila siku huduma za umma zinaendelea kulengwa na makombora nchini Syria, na hivyo kuvunjwa kwa sheria ya kimataifa kuhusu vita.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imesema kwamba mashambulizi ya makombora yaliyoharibu kiwanda cha kusafishia maji mjini Aleppo nchini humo wiki iliyopita ni mfano wa vitendo hivyo.

UNICEF imeeleza kwamba mashambulizi hayo yamesitisha huduma za maji kwa watu wapatao milioni 3.5, kiwanda hicho kikiwa kinatoa lita milioni 18 za maji ya kunywa kila siku.

Kwa mantiki hiyo UNICEF imekumbusha kwamba sheria ya kimataifa ya kibinadamu inalinda miundombinu ya umma na haki za raia kupata huduma hizo, shirika hilo likikariri wito wake kwa pande za mzozo wa kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya maji.