Maelfu ya watu wapata uraia Thailand

Maelfu ya watu wapata uraia Thailand

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limekaribisha uamuzi wa serikali ya Thailand wa kuwapatia uraia watu 18,000 waliokuwa wamekosa utaifa, likisema ni hatua kubwa kwenye kampeni ya kutokomeza ukosefu wa utaifa ifikapo mwaka 2024.

Hata hivyo bado idadi ya watu waliokosa utaifa nchini Thailand ni zaidi ya 400,000, wengi wao wakiwa wamekosa uhusiano na nchi zao za asili au wametoka makabila yanayoishi kwenye maeneo ya milima yaliyo mpakani mwa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR William Spindler ameelezea juhudi za UNHCR katika kusaidia serikali ya Thailand akimulika changamoto zinazokumba watu wasiokuwa na utaifa.

(Sauti ya Bwana Spindler)

« Bila uraia, wengi wanasema kwamba hawawezi kupata haki zao za binadamu ikiwemo ile ya kutembea kwa uhuru na kumiliki ardhi. Mara nyingi wanakosa huduma za msingi kama vile afya au elimu ya ngazi ya juu. Fursa za kazi zinakuwa chache kwa sababu ya kuzuiliwa kutembea na kusoma. »

Ikisema kwamba Thailand ni mfano wa kuiga kwa ukanda mzima, UNHCR imekumbusha kwamba zaidi ya watu milioni 10 wamekosa uraia duniani kote, asilimia 40 wakiishi barani Asia.