Burundi hakuna mashauriano ya dhati baina ya pande kinzani

Burundi hakuna mashauriano ya dhati baina ya pande kinzani

Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanapanga safari ya kwenda Burundi wakati huu ambapo wameelezwa kuwa serikali ya nchi hiyo haitoi ushirikiano kwa msuluhishi wa Muunganowa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Taarifa hizo zimetolewa kufuatia kikao cha faragha kuhusu Burundi ambapo mshauri mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo Jamal Benomar amewaeleza wajumbe kuwa hakuna mazungumzo ya dhati baina ya pande kinzani  na hivyo ni vyema kuimarisha uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Punde baada ya kikao hicho Bwana Benomar alizungumza na waandishi wa habari na kusema..

(Sauti ya  Benomar)

“Mzozo wa sasa Burundi hauwezi kusuluhishiwa kijeshi. Pande zote zinapaswa kuwajibika kwa ajili ya amani na utulivu nchini  humo,  kukataa kabisa ghasia na kushiriki katika mchakato shirikishi na halali wa kisiasa. Umoja wa Mataifa unasalia tayari kutumia njia zote ambazo zinaweza kurejesha amani nchini humo na una utaalamu wa kutosha kwenye eneo hilo. Tuko tayari kusaidia Burundi na wananchi wake kwa kuzingatia uamuzi wa Baraza la Usalama.”