Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Burundi bado si shwari, serikali haitoi ushirikiano kwa wasuluhishi:Baraza

Hali ya Burundi bado si shwari, serikali haitoi ushirikiano kwa wasuluhishi:Baraza

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha faragha kuhusu Burundi ambapo mshauri maalum wa Katibu Mkuu nchini humo Jamal Benomar amewaeleza wajumbe kuhusu hali ilivyo nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Matthew Rycroft ambaye ndiye Rais wa Baraza la usalama la Usalama kwa mwezi wa Novemba amesema kwa ujumla wajumbe baada ya taarifa hiyo wamekubaliana kuwa hali haitii matumaini huku ukiukwaji wa haki za binadamu ukiendelea.

(Sauti ya Balozi Rycroft)

“Hali bado si nzuri nchini humo na kuna ripoti zaidi za ghasia, na kuna maendeleo madogo katika mazungumzo. Bwana Benomar amesisitiza umuhimu wa uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi kusaidia michakato ya kisiasa na kiusalama.”

Alipoulizwa kuhusu hali ya sasa na hatua ambazo Baraza linaweza kuchukua, Balozi Rycroft amesema..

(Sauti ya Balozi Rycroft)

Bwana Benomar katika taarifa yake amesema hakuna mazungumzo ya dhati na serikali ya Burundi imekuwa haitoi ushirikiano kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ni msuluhishi wa Muungano wa Afrika na Jumuiya ya Afrika hivyo ni lazima tushinikize pande zote kwenye mwelekeo huo na tutatumia mbinu za kidipomasia ikiwemo mashauriano na pia dunia kuangazia nchi hiyo ili serikali itambue kuwe dunia inatazama na isitumie fursa yoyote kuendelea na ukiukaji wa haki za binadamu.”

Rais huyo wa Baraza la usalama amesema wajumbe wamekubaliana kupanga safari ya kwenda Burundi ambapo Marekani ambayo ndiyo inachukua nafasi ya urais kwa mwezi Disemba itaratibu suala hilo.