Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mashambulizi ya ADF dhidi ya MONUSCO

Ban alaani mashambulizi ya ADF dhidi ya MONUSCO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi yaliyofanyika na waasi wa ADF nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC dhidi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imeeleza kwamba katika shambulio hilo la Jumapili huko Makembi, jimbo la Kivu Kaskazini, mlinda amani mmoja kutoka Malawi aliuawa na mwingine kujeruhiwa.

Halikadhalika wanajeshi wengine wanne wa jeshi la kitaifa la DRC na raia kadhaa waliuawa siku hiyo hiyo kwenye mashambulizi mengine yaliyofanywa na ADF.

Katibu Mkuu ameomba watekelezaji wa mashambulizi hayo wafikishwe mbele ya sheria akielezea wasiwasi wake juu ya ongezeko la idadi ya mashambulizi yanayotekelezwa na waasi wa ADF ambapo zaidi ya raia 500 wameuawa tangu Oktoba mwaka 2014.

Bwana Ban ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga, serikali na raia wa Malawi, akiwatakia nafuu waliojeruhiwa, na kukariri msimamo wa MONUSCO kuisaidia serikali ya DRC kupambana na vikundi vilivyojihami nchini humo.