Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#COP21: Ushirika wa kimataifa wa matumizi ya nishati ya jua wazinduliwa

#COP21: Ushirika wa kimataifa wa matumizi ya nishati ya jua wazinduliwa

Huko Paris, Ufaransa kumefanyika uzinduzi wa ushirika wa kimataifa wa matumizi ya nishati ya jua, International Solar Alliance ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ni fursa pekee kwa nchi zenye utajiri wa nishati hiyo kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Ban amesema moja ya malengo ya maendeleo endelevu ni kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ambapo nishati endelevu kama hiyo ya jua ni mojawapo ya misingi yake.

Kwa mantiki hiyo amesema nchi zinazoendelea lakini tajiri wa nishati ya jua zinaweza kuimarisha uhakika wao wa kupata nishati endelevu hadi kwa watu maskini na hivyo kupunguza gharama za uagizaji nishati kutoka nje sambamba na nishati zinazotoa gesi chafuzi.

Ban amemshukuru Waziri Mkuu Narendra Modi wa India na serikali ya nchi hiyo kwa kuanzisha ushirika huo akitaka jamii ya kimataifa hususan nchi zilizoendelea kusaidia katika usaidizi wa teknolojia na fedha ili kupanua wigo wa matumizi ya nishati hiyo.