Skip to main content

Nchini Nepal manusura wa matetemeko ya ardhi kukumbwa na janga la afya

Nchini Nepal manusura wa matetemeko ya ardhi kukumbwa na janga la afya

Zaidi ya watoto milioni tatu wenye umri wa chini ya miaka mitano wako hatarini kufariki dunia au kukumbwa na magonjwa nchini Nepal wakati wa msimu wa baridi.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF ambalo limesema kwamba machafuko yanayotokea kusini mwa nchi hii kutokana na mvutano juu ya suala la katiba mpya yamekwamisha bidhaa kama vile mafuta, chakula, madawa na chanjo kuingizwa kupitia mpakani.

Tayari maduka ya serikali yamekumbwa na ukosefu wa chanjo dhidi ya kifua kikuu na akiba ya antibiotiki ni ndogo.

Kwenye taarifa yake UNICEF imeonya kwamba watoto wako hatarini zaidi kuathirika na hali hii, hasa wale waliopoteza makazi yao katika matetemeko ya ardhi ya mwezi April na Mei mwaka huu, ambao wengi wao bado wanaishi kwenye mahema ya muda, katika milima ambapo halijoto inakuwa ya baridi sana wakati wa msimu wa baridi.