Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Francis ahitimisha ziara CAR

Papa Francis ahitimisha ziara CAR

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis, amehitimisha ziara yake huko Jamhuri ya Afrika ya kati ikiwa ni nchi ya mwisho kutembelea katika ziara yake barani Afrika.. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Nats...

Moja ya shamrashamra kwa Papa Francis wakati akiwa huko Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati siku ya jumapili.

Ziara hiyo ilimpeleka kwenye moja ya misikiti kuzungumza na viongozi wa dini ya kiislamu, pamoja na kutembelea kambi ya wakimbizi wa ndani ya Saint Sauveur mjini Bangui. Halikadhalika alifika ikulu kwa mazungumzo na Rais wa CAR Catherine Samba-Panza,  na hatimaye alizungumza na waandishi wa habari akatoa ujumbe wa maridhiano akisema :

¨ Wakati ambapo Jamhuri ya Afrika ya Kati inaelekea taratibu kupata utulivu licha ya changamoto za kisiasa na kijamii, niko kwenu kwa mara ya kwanza baada ya aliyenitangulia, Baba mtakatifu Yohaba Paul wa Pili. Nakuja kama hija wa amani. »

Kwa upande wake Rais wa Samba-Panza ameeleza kufurahishwa na uwepo wa Papa Francis nchini humo akisema ni dalili ya kufanikiwa kwa imani na mshikamano dhidi ya uoga na mivutano nchini humo.