Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia imekutana kukabili kitisho cha pamoja:UNEP

Dunia imekutana kukabili kitisho cha pamoja:UNEP

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP Achim Steiner akizungumza kwenye mkutano wa 21 wa mabadiliko ya tabianchi, COP21 huko Paris, Ufaransa amesema viongozi wa dunia wamekutana kukabiliana na janga linalotishia ulimwengu mzima.

Amewaeleza washiriki  kuwa mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa ya zama za sasa na hivyo lazima wajumbe wa mkutano huo watumie fursa iliyopo kuchagiza hatua za kudhibiti ongezeko la joto duniani kuliko ilivyokuwa awali, akitaja zaidi uongozi wa ngazi ya juu zaidi upitishe maamuzi thabiti.

Naye Katibu Mtendaji wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC Christiana Figueres amesema macho ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote yameelekezwa Paris wakiwa na matumaini kwa viongozi wa dunia.

Amesema viongozi hao siyo tu wana fursa bali pia na wajibu wa kuhitimisha makubaliano ambayo yatawezesha kufanikisha malengo ya kitaifa yatakayosaidia nchi zinazoendelea na kuweka matumaini kwa ulimwengu mzima.