Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagonjwa zaidi wa kipindupindu Tanzania:WHO

Wagonjwa zaidi wa kipindupindu Tanzania:WHO

Idadi ya watu waliofariki dunia nchini Tanzania kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu imeongezeka na kufikia 150 sambamba na wagonjwa waliothibitishwa kuwa ni 9,871.

Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya nchini humo kwenda wa shirika la afya duniani, WHO ambapo hadi tarehe 25 mwezi huu ugonjwa huo umekumba mikoa 19, Dar es salaam ikiwa na wagonjwa wengi zaidi.

Kipindupindu kimeripotiwa pia Zanzibar kwenye visiwa vya Pemba na Unguja ambapo hata hivyo licha ya kwamba idadi ya visa vipya kwa siku inapungua, wasiwasi sasa ni mvua za El Nino ambazo zinaelezwa zinaweza kusababisha mafuriko na ugonjwa kuenea zaidi.

WHO imesema inaendelea kushirikiana na wadau wa afya kupitia kikosi kazi maalum kilichoundwa kuhakikisha ufuatiliaji, utabibu na kuelimisha umma kuhusu kanuni za usafi.

Kipindupindu kiliripotiwa Dar es salaam mwezi Julai mwaka huu na kuenea katika mikoa mingine.