Akiwa Nairobi, Pope Francis awageukia viongozi kuhusu COP21

Akiwa Nairobi, Pope Francis awageukia viongozi kuhusu COP21

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Pope Francis akianza hotuba yake mbele ya hadhara iliyojumuisha viongozi wa Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya sanjari na wanadiplomasia.

Hapa ni Gigiri ambapo Pope Francis baada ya kutembezwa kwenye ofisi za shirika la mazingira duniani, UNEP na kukabidhiwa sanamu ya tembo iliyotengenezwa na mabaki ya taka, ametaka viongozi duniani kuridhia makubaliano thabiti wakati wa COP21 huko Paris, Ufaransa.

Papa Francis amesema suala la mabadiliko ya miundo ya sasa ya maendeleo linataka wajibu wa kiuchumi na kisiasa na kwa mantiki hiyo amependekeza kuridhiwa kwa mifumo ya kiuchumi inayotoa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa.

Halikadhalika ametaka jamii kuachana kabisa na utamaduni wa kutupa hovyo vyakula kwani husababisha gesi chafuzi aina ya Methane.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi, Sahle-Work Zewde, alipongeza hatua za Papa Francis za kupigia chepuo mbinu sahihi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi huku Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Achim Steiner katika hotuba yake akipongeza uongozi wa Papa Francis katika suala la mazingira.

(Sauti Steiner )

Kupitia waraka wako mkuu, Laudato Si, kuhusu mazingira na hivi karibuni zaidi hotuba yako kwenye baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa, umeeneza dira yako ya dunia ambamo kwayo binadamu na viumbe vingine kwenye mazingira wanaweza kuishi kwa amani. Motisha huo unatuongoza kwenye uelewa wa wajibu wetu kwa kila mtu na kwa sayari yetu ambayo leo inapatia makazi watu Bilioni Saba lakini punde itatakiwa kuhifadhi watu Bilioni Tisa.”

Kutoka Kenya, hapo kesho, Papa Francis ataelekea Uganda na hatimaye Jamhuri ya Afrika ya Kati