Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yachangia juhudi dhidi ya ukatili wa kijinsia

WHO yachangia juhudi dhidi ya ukatili wa kijinsia

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake, Shirika la Afya Duniani WHO limezindua leo mradi mpya wa kusaidia nchi kuimarisha uwezo wao wa kufuatilia watekelezaji wa ukatili huo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WHO imelaani aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuziunga mkono juhudi za nchi katika kupambana na aina hiyo ya ukatili.

Mradi wa WHO unalenga kusaidia nchi kuimarisha uwezo wao wa kuchunguza kesi za ukatili kupitia viwango na miongozo kuhusu namna ya kuendesha uchunguzi wa aina hiyo.

Taarifa ya WHO imesisitiza kwamba uchunguzi wa dhati ni lazima ili kutokomeza ukwepaji sheria na kuwatendea haki wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Aidha WHO imeeleza kwamba wanawake wanaofanywa ukatili wa mume zao wako hatarini kukumbwa na udhoofu , magonjwa ya zinaa, kuharibika kwa mimba au uzazimfu. Kwa hiyo WHO pia inatoa huduma za afya, ikiwemo ya afya ya akili ili kusaidia wanawake wahanga wa ukatili wa kijinsia.