Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2015 kuvunja rekodi ya kuwa na joto zaidi: WMO

Mwaka 2015 kuvunja rekodi ya kuwa na joto zaidi: WMO

Kuelekea mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa COP21, shirika la hali ya hewa duniani, WMO limesema mwaka huu wa 2015 utaingia katika historia kutokana na kuwa na kiwango cha juu zaidi cha joto duniani tangu kuanza kuwekwa kwa kumbukumbu za hali ya hewa.

Katibu Mkuu wa WMO Michel Jarraud amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa wastani wa ongezeko la joto mwaka huu utakuwa nyuzi joto moja zaidi katika kipimo cha selsiyasi kulinganisha na mwishoni mwa karne ya 19.

Sababu alizotaja ni mchanganyiko wa El nino na shughuli za binadamu zinazochochea ongezeko la joto duniani na hivyo ameonya kuwa..

(Sauti ya Jarraud)

Tayari tumeshalipatia anga joto kwa zaidi ya asilimia 50 ya kiwango kinachotakiwa. Na hili ni jambo linalotutia wasiwasi mkubwa kwa kuwa kama  tulivyosema awali hewa yoyote chafuzi iliyokwenda angani inasalia hapo kwa muda mrefu, kuanzia  miongo na karne! Kwa hiyo hatuna muda.”

Katika ripoti hiyo WMO pia imesema kwa tathmini ya miaka mitano mitano, kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 nacho kitavunja rekodi ya kuwa na joto zaidi.