Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aelezea matarajio yake kwa COP21

Ban aelezea matarajio yake kwa COP21

Siku nne kabla ya kuanza kwa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP21 huko Paris, Ufaransa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mafanikio ya mkutano huo  yako mikononi mwa viongozi wa dunia.

Katika tahariri yake iliyochapishwa leo kwenye magazeti mbali mbali ikiwemo The Citizen nchini Tanzania, Daily Nations Kenya na Daily Monitor huko Uganda, Ban amesema ni kwa mantiki hiyo  viongozi hao wanapaswa kuangalia zaidi ya maslahi ya nchi zao na badala yake walegeze misimamo na kufikia maridhiano katika masuala yenye mvutano ikiwemo uwiano tofauti katika uwajibikaji wa nchi na uchangiaji fedha kwa mujibu wa kiwango cha uchafuzi.

Ban amesema mafanikio hayawezi kupatikana mara moja na kwamba mkutano wa Paris siyo ukomo bali ni mwanzo wa safari yenye matumaini katika kupunguza utoaji gesi chafuzi na kujenga mustakhbali unaoweza kukabiliana na mazingira.

Hivyo amesema anataraji mkataba huo uwe na mambo makuu manne ikiwemo mazingira ya kwenda na wakati, uhalali na mshikamano katika kukabili mabadiliko ya tabianchi na kwamba Umoja wa Mataifa unasalia tayari kuunga mkono mataifa katika kutekeleza mkataba wa aina hiyo.