Skip to main content

UM na kutunguliwa kwa ndege ya Urusi

UM na kutunguliwa kwa ndege ya Urusi

Siku chache baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha kwa kauli moja azimio la kuimarisha harakati dhidi ya kikundi cha kigaidi cha ISIL, ripoti kwamba Uturuki imetungua ndege ya Urusi iliyokuwa katika harakati za kukabiliana na kikundi hicho zinaelezwa kuongeza mkanganyiko kwenye sakata hilo. Amina Hassan na ripoti kamili.

(Taarifa ya Amina)

Akijibu swali la mwandishi wa habari kwenye mkutano huko Geneva, Uswisi, aliyetaka kufahamu mustakhbali wa operesheni dhidi ya ISIL katika mazingira hayo, Ahmed Faqzi ambaye ni msemaji wa Umoja wa Mataifa huko Geneva amesema ni kweli anafahamu kuhusu suala la ndege ya Urusi kutunguliwa na Uturuki kwenye mpaka wake na Syria.

(Sauti ya Fawzi)

"Uturuki imetangaza kuwa imetungua ndege ya Urusi na hii itafanya mambo kuwa magumu zaidi. Kama ulivyosema sahihi, Baraza la Usalama limepitisha maazimio ya kukabili ugaidi na nafiriki sote tunataka kuona ugaidi unatokomezwa kwenye eneo hilo na katika maisha yetu. Na kwa mantiki hiyo mataifa yameamua yatatumia mbinu zote kufanya hivyo. Lakini kile alichosisitiza Katibu Mkuu ni kwamba ni lazima tuzingatie sheria za kimataifa za kibinadamu na si kukiuka maadili ya haki za binadamu.”

Wakati huo huo, Kamati dhidi ya ugaidi ya Baraza la Usalama imekuwa na kikao leo kuchambua kuibuka kwa magaidi mamluki ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo amerejelea kauli ya Baraza hilo kuwa ugaidi hauhalalishiki katika mazingira yoyote yale.