Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapalestina wamechoka kusubiri kutendewa haki: Umoja wa Mataifa

Wapalestina wamechoka kusubiri kutendewa haki: Umoja wa Mataifa

Wakati wa kuelekea siku ya kimataifa ya kuonyesha mshikamano na raia wa Palestina tarehe 29 mwezi huu, mjadala maalum kuhusu swala la Palestina umefanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ukishirikiwa wawakilishi wa Umoja huo, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa Palestina na wa jamii. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Raia wa Palestina wamechoka kusubiri, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft, akihutubia mkutano huo, akiongeza kwamba haki za msingi za wapalestina hazijatimizwa.

Amesema tangu 1967  Baraza Kuu linalaani utawala wa Israel kwenye maeneo ya Palestina ambao ni kinyume na haki, akisema kitendo hicho kinazidi kuchochea ghasia kwenye ukanda mzima. Hivyo amechukua fursa ya leo kukariri wito wa baraza hilo.

(Sauti ya Bwana Lykketoft)

Suluhu endelevu kwa mzozo huo unaoendelea kwa muda mrefu inapaswa kupatikana. Kuendelea kukaliwa kwa maeneo ya palestina kunapaswa kusitishwa bila kuchelewa, ili kuanzisha taifa la Palestina litakalokuwa sambamba na  taifa la Israel kwa amani na usalama kwenye mipaka itakayotambuliwa kwa misingi ya mipaka ya 1967.”   

Siku ya kimataifa ya mshikamano na raia wa Palestina huadhimishwa kila mwaka tangu 1977 ili kuadhimisha azimio 181 la mwaka 1947 la Baraza hilo kuhusu kugawanyika kwa Palestina.