Skip to main content

Nigeria sitisha bomoa bomoa inayoendelea Lagos:Mtaalamu

Nigeria sitisha bomoa bomoa inayoendelea Lagos:Mtaalamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu  haki ya kuwa na malazi ya kutosha, Leilani Farha, ameitaka serikali ya Nigeria kusitisha mwelekeo wa sasa wa bomoabomoa na kuwafurusha watu kwenye makazi yao. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Ametoa kauli hiyo kufuatia bomoa bomoa inayoendelea kwenye eneo la Badia lililoko mji wa Lagos nchini humo ambayo imesababisha maelfu ya watu kusalia bila makazi.

Amesema anatiwa hofu kwa kuwa zaidi ya watu Elfu Kumi wakiwemo watoto, wanawake na wazee wamefurushwa makwao bila notisi yoyote wakati huu ambapo ni msimu wa mvua na polisi wakiwa mstari wa mbele kushinikiza zoezi hilo.

Bi. Farha amesema zoezi la namna hiyo la mwaka 2013 huko Lagos, nalo pia lilikiuka sheria na mtu mmoja kati ya watatu waliofurushwa hadi sasa hawana makazi.

Kwa mantiki hiyo mtaalamu huyo ametaka serikali ya Nigeria kusitisha mara moja bomoabomoa hiyo inayoendeshwa kinyume cha sheria huku akitaka wale ambao wameshakumbwa nayo walipwe fidia.