Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumalizika mzozo Syria, ni ushindi dhidi ya ISIL:Baraza

Kumalizika mzozo Syria, ni ushindi dhidi ya ISIL:Baraza

Baraza la usalama la  Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limepitisha azimio dhidi ya kikundi cha kigaidi cha ISIL huku likisema kuwa hali ya usalama na amani duniani itazidi kuzorota zaidi iwapo hakuna suluhu kwenye mzozo wa Syria.

Kwa mantiki hiyo azimio hilo namba 2249, limesisitiza umuhimu wa kutekeleza tamko la pamoja la Geneva la tarehe 30 Juni mwaka 2012 linalotambuliwa pia kama azimio namba 2118 la mwaka 2013 na tamko la pamoja la pili la Vienna la tarehe 14 Novemba mwaka 2015.

Wajumbe pia wametumia fursa hiyo kulaani vikali mashambulio mbali mbali ya kigaidi yaliyofanywa na ISIL kwenye maeneo mbali mbali duniani ikwiemo Sousse, Ankara, Sinai, Beirut na Paris na kusema kusema ISIL inaweza na ina nia ya kufanya mashambulizi zaidi na kwamba vitendo hivyo vyote ni ugaidi na ni tishio kwa amani na usalama duniani.

Wametaka wahusika wa mashambulio  hayo wawajibishwe na nchi zenye uwezo wa kufanya hivyo zichukue hatua kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu.

Halikadhalika wameeleza nia yao ya kufanyia marekebisho orodha ya vikwazo ili kuakisi vitisho vinavyoweza kusababishwa na ISIL ijulikanayo pia kama Da’esh.

Azimio hilo lilipendekezwa na Ufaransa ambayo mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi François Delattre ametoa ufafanuzi baada ya kupitishwa..

(Sauti ya Balozi Delattre)

 “Azimio hili linadhibiti hatua zetu kwenye mfumo wa haki ya kimataifa na katiba ya Umoja wa Mataifa ambao ni manufaa ya umma, naweza kusema ni hazina yetu. Pia ni njia ya kupambana kwa ufanisi dhidi ya ugaidi wa kimataifa. Mashambulizi ya Novemba 13 ni chokochoko ya vita dhidi ya Ufaransa.”