Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanateseka ,wanusuriwe: Ban

Watoto wanateseka ,wanusuriwe: Ban

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya watoto, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameitaka jumuiya ya kimataifa kuhakikisha ahadi zao kwa watoto zinaelekezwa husuani kwa kundi ambalo mara nyingi husahaulika na hunyimwa uhuru wao.Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya watoto inayoadhimishwa Novemba 20 kila mwaka, Ban amesema kundi hilo linakumbana na madhila kadhaa ikiwamo kusota magerezani, kushikiliwa katika vituo vya kutibu afya ya akili na aina nyingine za uwekwaji korokoroni. Hivyo ametaka maslahi ya watoto yatimizwe ikiwamo ulinzi dhidi ya uhuru wao.

Wakati huo huo mashirika  ya Umoja wa Mtaifa likiwamo la kuhudumia watoto UNICEF na ofisi ya UM ya misaada ya kibinadamu OCHA yamesisitiza kuwa watoto huteseka kwa kukosa elimu kutokana na migogoro inayoendelea duniani mathalani barani Ulaya ambako wimbi la wakimbizi na wahamiaji limewaathiri . Takwimu zinaonyesha kuwa watoto 700 kila siku huingia barani humo wakisaka hifadhi.

Jens Larke ni msemaji wa OCHA mjini Geneva..

(SAUTI LARKE)

“Mzozo ni jinamizi hai, kwa kila mtu, hasa watoto. Unawaharibia utoto wao na mustakhabali wao. Tunakaribia sana kupoteza kizazi kizima katika uoga, ujinga wa kutojua kusoma na kuandika na giza.”