Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la kigaidi Bamako, MINUSMA yasaidia wahanga

Shambulio la kigaidi Bamako, MINUSMA yasaidia wahanga

Nchini Mali kwenye mji mkuu Bamako kumefanyika shambulio la kigaidi ambako watu kadhaa yaripotiwa kushikiliwa na washambuliaji wenye silaha. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Vyanzo vya habari vinasema shambulio hilo kwenye hoteli Raddison Blu, mjini Bamako limefanyika Ijumaa ambapo Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa umoja huo nchini Mali Mongi Hamdi amelaani vikali.

Katika taarifa yake, Hamdi ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA amesema wanachofanya sasa ni kusaidia vikosi vya serikali kuimarisha usalama, kuokoa wanaoshikiliwa sambamba na majeruhi kwenye eneo la tukio.

Bwana Hamdi ameelezea mshikamano wake na wote waliokumbwa na kisa hicho.

Mwandishi wa Habari Karim Djinko kutoka Redio ya Umoja wa Mataifa Mikado FM nchini Mali amesema:

(Sauti ya Bwana Djinko)

" Shambulio limeanza saa 1 za asubuhi na polisi wameanza kuvamia saa 3 saa za Bamako, na vitu vingi vimetokea tangu saa zile na tayari watu 15 wamefariki dunia, na bahati mbaya matokeo yanaweza kuwa mabaya zaidi. Magari ya wagonjwa ya MINUSMA yamekuja kusaidia majeruhi na timu za MINUSMA ziko kila sehemu."