Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumaini yapo kuhusu sitisho la mapigano Syria: De Mistura

Matumaini yapo kuhusu sitisho la mapigano Syria: De Mistura

Sitisho la mapigano kwa ngazi ya kitaifa nchini Syria linawezekana sasa, amesema leo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo wa Syria, Staffan de Mistura, akitaja sababu kuwa nchi zote zinazohusishwa kwenye mapigano zimeanza kuona faida inayoweza kupatikana kwenye utekelezaji wa sitisho hilo, hasa mwelekeo wa kisiasa.

Bwana de Mistura amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa faragha kuhusu mzozo wa Syria na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo hazikuhudhuria mjadala uliofanyika wiki iliyopita kwenye Baraza la Usalama kuhusu mada hiyo.

Ameongeza kwamba pande zote za mzozo zinaweza kutekeleza sitisho hilo, isipokuwa waasi wa ISIS ambao hawakushiriki mazungumzo ya amani yaliyofanyika mjini Vienna, Austria.

Aidha Bwana de Mistura amesema kwamba yaliyozungumzwa Vienna ni maswala ya msingi ambayo yameweza kuridhisha serikali pamoja na wawakilishi wa upinzani.

(Sauti ya bwana de Mistura)

" Tunazungumzia kuhusu utawala jumuishi ambao utaaminika na hautambagua mtu yeyote. Pia tunazungumzia katiba mpya, na uchaguzi, na wala si uchaguzi wa wabunge tu. Ni mambo mengi, ambayo yanaweza kuvutia upinzani ambao haukuridhika."