Skip to main content

Fahamu kuhusu mkutano wa tabianchi COP21

Fahamu kuhusu mkutano wa tabianchi COP21

Kwa nini mkutano wa Tabianchi la Paris linaitwa COP21 ? 

Ni kongamano la 21 la nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Mkataba huo ulisainiwa kwenye kongamano la dunia la Rio mwaka 1992 na kuridhiwa na nchi 195 mwaka 1994. Pia kongamano hilo ni mkutano wa 11 wa nchi wanachama wa mkataba wa Kyoto kuhusu kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.

Nani atahudhuria COP21 ?

Watu wapatao 45,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo utakaoanza tarehe 30, Novemba hadi Disemba tarehe 11 mwaka huu wa 2015. Na mkutano utafanyika eneo liitwalo Le Bourget, kwenye viunga vya mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Ni matokeo gani yanayotarajiwa?

Kuna mambo makubwa matatu:

Mosi; Ni makubaliano ambayo yatakuwa na nguvu kisheria kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Pili; Ni mwafaka kuhusu michango ya mambo yanayotarijiwa kutekelezwa kitaifa (INDCs). Kila nchi mwanachama inatarajiwa kutangaza mchango wake na kuutekeleza.

Na tatu ni mpango wa ufadhili ili kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza makubaliano hayo.

Nchi ngapi zimeshatangaza michango yao ?

Kufikia tarehe 31, Oktoba mwaka huu, tayari nchi 155 zimeshatangaza michango yao ya kitaifa, ikiwa ni sawa na asilimia 90 ya uzalishaji wote wa gesi chafuzi duniani. Nchi zote za Afrika Mashariki zimeshatangaza michango yao.

Na kuna tovuti inayorodhesha nchi zote na michango yao.

Michango ya nchi za Afrika ni ya aina gani ?

Michango ya nchi za Afrika inahusu sekta zote za uchumi, kama vile kilimo, ufugaji, misitu, uvuvi, utalii, nishati au afya.

Kwa mfano Tanzania imeahidi hatua 30 tofauti ikiwemo kuimarisha matumizi ya maji na ardhi katika shughuli za kilimo, na kusaidia jamii zinazoishi karibu ya pwani na yanayoweza kuathiriwa na ongezeko la kiwango cha bahari.

Kwa upande wake Rwanda imetangaza miradi 20 ikiwemo kukuza matumizi ya mbolea na usindikajii wa maji machafu kwenye sekta ya kilimo, pia kuunda mfumo wa usafiri wa umma mijini.

Mpango wa ufadhili unafananaje ?

Nchi wanachama zimeshaahidi kutoa dola bilioni 100 kila mwaka hadi mwaka 2020 ili kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hadi sasa, baadhi ya fedha hizo zimepatikana lakini si zote. Mpango wa ufadhili utaonyesha jinsi ya kupata hizo fedha na kuwezesha nchi zinazoendelea kutafuta mbinu ili kufadhili zenyewe jitihada zao baada ya mwaka 2020.

Kwa nini ni muhimu kudhibiti ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi mbili za joto kwenye kipimo cha selisiasi ?

Tayari uchafuzi wa mazingira na uzalishaji wa gesi chafuzi umesababisha ongezeko la nyuzi 0.85 za Selisiadi tangu mwaka 1880. Ongezeko hilo limesababisha matokeo makubwa mabaya yakiwemo kuyeyuka kwa nusu ya barafu duniani, kupanda kwa kiwango cha bahari na kufa kwa mamilioni ya miti kwa sababu ya magonjwa yaliyosababishwa na joto.

Watalaam wa jopo la kiserikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC wamesema kwamba, iwapo hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa, joto litakuwa limeongezeka kwa nyuzi nne hadi sita ifikapo mwaka 2100, na hivyo kusababisha idadi kubwa zaidi ya majanga duniani kote, kama vile ukame, mafuriko, ukosefu wa maji. Litasababisha pia maji ya bahari kuchachuka zaidi na hivyo kuhatarisha uwepo wa aina nyingi za samaki na viumbe vingine, pamoja na kutoweka kwa mwamba unaolinda maeneo mengi duniani ikiwemo Zanzibar kwa mfano.

Mwaka 2009 mjini Copenhagen,Denmark na nchi wanachama wa mkataba kuhusu mabadiliko ya tabianchi ziliamua kudhibiti ongezeko hilo ili lisizidi nyuzi mbili ifikapo 2100.

Je inawezekana kufikia lengo hilo ?

Ili kutimiza ahadi hiyo, watalaam wa IPCC wamesema itabidi kupunguza kwa kati ya asilimia 40 hadi 70 uzalishaji wa gesi chafuzi angani ifikapo mwaka 2050.

Hadi sasa, michango iliyoahidiwa ikitekelezwa, ongezeko la halijoto litakuwa la nyuzi tatu ifikapo mwisho wa karne hii. Kwa hiyo, itabidi nchi wanachama ziongeze bidii ili kupunguza zaidi uzalishaji wa gesi chafuzi. Makubaliano ya Paris yanatarajiwa pia kuunda mchakato wa tathmini kila baada ya miaka mitano ili kuimarisha jitihada za nchi zote.