Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafanikio makubwa yapatikana dhidi ya Malaria

Mafanikio makubwa yapatikana dhidi ya Malaria

Lengo namba sita la kupunguza Malaria kwa asilimia 50 kwa mujibu wa malengo ya maendeleo ya Milenia, MDG limefanikiwa kupita kiasi.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mpango wa kutokomeza malaria duniani, Roll Back Malaria ikitolea mfano barani Afrika ambako asilimia 97 ya vifo vitokanavyo na Malaria vimeepukika.

Taarifa hiyo imetolewa ikiwa jioni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft ataungana na viongozi wengine kutambua mafanikio hayo ambapo amesema ni ishara kuwa mshikamano na ubia ni silaha katika kuleta mafanikio.

Imetaja pia zaidi ya nchi 100 ambazo kwazo ugonjwa wa malaria umesalia historia ilhali nchi nyingine 55 ziko katika mwelekeo wa kupunguza kwa asilimia 75 visa vya ugonjwa huo hatari.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ubia na uratibu maridadi kupitia Robb Back Malaria na ongezeko la uchangishaji fedha vimesaidia kupunguza kwa zaidi ya asilimia 50 tangu mwaka 2000 vifo vitokanavyo na Malaria.

Licha ya mafanikio hayo, shirika la afya duniani, WHO linakadiria kuwa bado Malaria ni tishio kwa baadhi ya maeneo ambako mwaka 2015 pekee kumeripotiwa visa zaidi ya Milioni 214 vya Malaria, na wahanga zaidi ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.