Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuua vijana wa Burundi ni kuua mustakhabali wa nchi: Dieng

Kuua vijana wa Burundi ni kuua mustakhabali wa nchi: Dieng

Mshauri Maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa mauaji wa kimbari Adama Dieng amesema mauaji ya vijana nchini Burundi ambao ni asilimia 75 ya raia wote, ni sawa na mauaji ya mustakhabali wa nchi.

Amesema hayo akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa baada ya kumaliza ziara yake nchini Burundi hivi karibuni ambako mauaji yanaripotiwa kila uchao.

Bwana Dieng amesema ingawa juhudi za jamii ya kimataifa ni muhimu katika kuafikiana suluhu ya kisiasa, ni wajibu wa raia wa Burundi wenyewe kushiriki mazungumzo ya pamoja ambayo yanapaswa kuwa jumishi na salama kwa wadau wote.

(Sauti ya Bwana Dieng)

“Tunachoshuhudia sasa Burundi ni kwamba ukabila unatumiwa vibaya na pande zote, serikali na upinzani. Tunajua kwamba matumizi hayo ni hatari. Yanaweza kutumika ili kuthonganisha na kuigawa jamii na hatimaye kuchochea chuki ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya sana.”

Bwana Dieng ametolea mfano hotuba ya rais wa baraza la seneti la Burundi akisema baadhi ya maneno yake yamefanana yale yaliyotumika Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari.

Amesisitiza kuwa mauaji ya aina hiyo hayapaswi kutokea tena akikumbusha kwamba watu 300,000 waliuawa Burundi kati ya mwaka 1993 na mwaka 2003 kwa sababu ya siasa za kibaguzi,