Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Grandi sasa rasmi kuongoza UNHCR

Grandi sasa rasmi kuongoza UNHCR

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limeridhia kwa kauli moja uteuzi wa Filippo Grandi kuwa Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Hatua hiyo imefuatia kikao kilichofanyika leo Jumatano kikiongozwa na Rais wa Baraza hilo Morgens Lykketoft kufuatia pendekezo la Katibu Mkuu Ban Ki-moon la kumteua Bwana Grandi kumrithi kamishna mkuu wa sasa Antonio Guterres aliyeongoza shirika hilo tangu mwaka mwezi Juni mwaka 2005.

Katika tangazo hili Bwana Lykketoft anahoji wajumbe kuwa achukulie kuwa Baraza limeridhia kumchagua Bwana Fillipo Grandi kuwa Kamishna Mkuu wa UNHCR kuanzia tarehe Mosi Januari 2015 kwa kipindi cha miaka Mitano hadi Disemba 2020.

Kimya kikatawala na ndipo akasema..

Imeamuliwa hivyo….

Ndipo wawakilishi mbalimbali wakapata fursa ya kuzungumza na miongoni mwao ni afisa kutoka ujumbe wa Muungano wa Ulaya, EU  kwenye Umoja wa Mataifa Jesus Diaz Carazo amempongeza Bwana Grandi akisema UNHCR ina dhima muhimu katika kulinda haki na ustawi kwa wakimbizi na watu wasio na utaifi.

“Kukiwa na watu Milioni 60 waliolazimika kukimbia makwao duniani kote kutokana na majanga mbali mbali duniani, baraza kuu limempatia jukumu Bwana Grandi kazikubwa ya kupaza sauti za wale walio hatarini. Katika muktadha huo, naomba niweke msisitizo kuwa EU na wanachama wake itaendelea kutoa usaidizi wa dhati kwa shirika hili kwa misingi ya ushirikiano wa kimataifa na mshikamano.”