Skip to main content

Ripoti mpya yabainisha fursa za kudhibiti ongezeko la joto duniani

Ripoti mpya yabainisha fursa za kudhibiti ongezeko la joto duniani

Ripoti mpya iliyosheheni mifano bora kutoka kote duniani ya mikakati na sera kuhusu tabianchi, imebainisha wingi wa fursa zilizopo za hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi mara moja, na hivyo kutoa msukumo kwa mtazamo kabambe wa kuhakikisha ongezeko la joto duniani halizidi nyuzi mbili kwenye kipimo cha Selisiasi.

Ripoti hiyo yenye kichwa, “Hatua kuhusu tabianchi sasa – muhtasari wa mwongozo kwa watunga sera 2015,” inamulika hatua za ushhirikiano kitaifa na kimataifa, ambazo tayari zinachukuliwa, huku ikiweka msisitizo kwa mchango wa serikali na kampuni, miji, na mikoa katika kupunguza uchafuzi wa hewa.

Ripoti imewasilishwa na Katibu Mtendaji wa Mkakati wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, Christiana Figueres mjini Bonn, Ujerumani, akisema

(Sauti ya Figueres)

Naweza kusema huu ni mwongozo na kitu kinachotia nguvu, kuelewa kuwa itakuwa bora tukifikia kati ya nyuzi joto 2.7 hadi Tatu, lakini tunapaswa kufanya juhudi zaidi, na kwamba juhudi hizo zinawezekana. Inawezekana kutekeleza sera hizi, na kwamba tayari nyingi tayari zinatekelezwa na zina matokeo mahsusi”

Ripoti inakuja siku chache kabla ya kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Tabianchi, ambalo litafanyika jijini Paris, Ufaransa kuanzia Novemba 30 hadi Disemba 11 mwaka huu, ambako serikali zitaafikia mkataba mpya jumuishi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.