Skip to main content

Hatma ya watoto Burundi mashakani:UNICEF

Hatma ya watoto Burundi mashakani:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeonya kuwa mustakhbali wa watoto nchini Burundi uko mashakani kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa AFrika, Leila Gharagozloo-Pakkala amesema hali hiyo inazingatia ukweli kwamba tangu kuanza kwa mzozo mwezi Aprili mwaka huu, watoto 17 wamefariki dunia ilihali wengine wengi wamejeruhiwa.

Amesema kama hiyo haitoshi, haki zao za msingi zinabinywa ikiwemo shule kuvamiwa akisema kuwa watoto hawapaswi kubeba gharama ya mzozo wa Burundi.

Bi. Gharagozloo-Pakkala amesema sheria za Burundi zimeweka bayana wajibu wa kuheshimu haki za watoto na kuwalinda dhidi ya ghasia na hivyo ni lazima sheria hizo ziheshimiwe.

Wakati hayo yakiendelea, imeripotiwa kuwa mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Uoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa mauaji ya halaiki Adama Dieng amehitimisha ziara Burundi kuona hali ilivyo.