Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itifaki dhidi ya utumikishaji kuanza kutumika mwakani:ILO

Itifaki dhidi ya utumikishaji kuanza kutumika mwakani:ILO

Norway imekuwa nchi ya pili baada ya Niger kuridhia itifaki ya mkataba wa kimataifa dhidi ya utumikishaji na hivyo kuwezesha itifaki hiyo kuanza kutumika tarehe Tisa Novemba mwakani.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kazi duniani, ILO Guy Ryder amesema hatua hiyo ya Norway ni muhimu kwa kuwa itasaidia mamilioni ya watoto, wanawake na wanaume ambao wamepoteza utu na hadhi yao kutokana na kutumikishwa kwenye ajira mbali mbali.

Halikadhalika amesema kuridhia kunawasilisha utashi thabiti wa kisiasa na ametoa wito kwa nchi nyingine kuchukua hatua hiyo ili kulinda wafanyakazi wanaotumikishwa.

Itifaki hiyo iliyoridhiwa na serikali za nchi wanachama wa ILO mwaka 2014 pamoja na mambo mengine ina vipengele kuhusu ulinzi dhidi ya utumikishwaji, kusaka haki na kutaka waajiri katika sekta ya umma na binafsi kuwa makini ili kuepuka utumwa wa kisasa kwenye sehemu zao za kazi.