WFP yapigwa jeki kuendelea kuwasaidia waathirika wa ukame Ethiopia

18 Novemba 2015

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limesema kuwa kufuatia ufadhili uliotolewa na wahisani wakuu, litaweza kuendelea kutoa msaada wa chakula kwa watu milioni 1.5 walioathiriwa na ukame katika jimbo la Somali nchini Ethiopia, na kuongeza usaidizi wa lishe kwa zaidi ya watoto laki saba na akina mama katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi.

WFP imesema kuongeza utoaji wa msaada wa chakula ni muhimu katika kuzuia watu walio hatarini kutumbukia katika mzozo mkubwa zaidi.

Hata hivyo, licha ya ufadhili huo mpya, WFP imesema ina asilimia saba tu ya bajeti ya dola milioni 228 zinazohitajika kutoa msaada wa chakula na lishe hadi mwezi Juni mwakani.

Ongezeko kubwa la watu wanaohitaji msaada wa chakula kutoka milioni 2.5 mwanzoni mwa mwaka hadi milioni 8.2 mwezi Oktoba, lilisababisha pengo kubwa la ufadhili, na hivyo WFP kuhofia mkwamo wa utoaji misaada kwa watu walioathiriwa na ukame mwishoni mwezi huu wa Novemba.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter