#WeProtect yaimarisha ubia wa serikali na kampuni kulinda watoto:UNICEF

#WeProtect yaimarisha ubia wa serikali na kampuni kulinda watoto:UNICEF

Kampuni kubwa za teknolojia kwa kushirikiana na serikali na mashirika ya kimataifa zimeazimia kulinda mamilioni ya watoto dhidi ya ukatili wa kingono kupitia mitandaoni.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hatua hiyo inatokana na mkutano wa ngazi ya juu ulioandaliaw na Falme za kiarabu na Uingereza huko Abu Dhabi.

Katika mkutano huo wa ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili wa kingono mitandaoni, serikali zimekubali kuweka mifumo ya kuratibiana baina ya sekta ya mahakama, polisi, watoa huduma za kijamii na sekta ya elimu ili kulinda kundi hilo.

Kwa upande wao kampuni za teknolojia zikiwemo Apple, Facebook, Google, Microsoft, Twitter na Yahoo zimeahidi kulinda watoto kwa kubuni teknolojia mpya, vifaa na kutoa utaalamu.

Akizungumzia hatua hiyo, Naibu Mkurugenzi wa UNICEF Fatoumata Ndiaye amesema ni kiashiria cha utashi wa kisiasa kutoka kona zote za dunia na wanaunga mkono kila nchi kuchukua hatua hiyo.

Hatua hiyo inakuja wakati huu ambapo tafiti zinaonyesha kiwango cha juu cha ukatili wa kingono dhidi ya watoto mitandaoni ambapo kati yam waka 2012 na 2014 matukio hayo yaliongezeka kwa asilimia 147.