Botswana ihakikishe inapatia maji raia wake: UM

Botswana ihakikishe inapatia maji raia wake: UM

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kupata maji safi ya kunywa, Léo Heller leo ameisihi serikali ya Botswana kutumia ukame unaokumba nchi hiyo hivi sasa kama fursa ya kuandaa mkakati thabiti wa kuhakikishia upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi kwa raia wote.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa leo baada ya ziara yake nchini Botswana, Bwana Heller amesema ukame huo usichukuliwe kama jambo la muda bali kichocheo cha kuweka uhakika wa upatikanaji maji kama kipaumbele cha taifa.

Amesema mchakato shirikishi wenye lengo la kupatia maji safi na salama kwa wote utakuwa njia fupi ya kuzuia hasara za kiuchumi pamoja na magonjwa, vifo vitokanavyo na matumizi ya maji machafu.

Bwana Heller amesema upatikanaji wa maji kwa wote bila ubaguzi wowote ni haki ya binadamu, huku akieleza kwamba ametembelea baadhi ya maeneo ya nchi ambapo hakuna huduma ya umma ya maji na wanawake na wasichana wanapaswa kutembea hadi kilomita moja ili kutafuta maji ambayo hata hivyo ni si salama.

Aidha Bwana Heller ameeleza kwamba ukosefu wa maji nchini humo unatarajiwa kuendelea kuongezeka.