Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa wito nchi zilinde afya kutokana na mabadiliko ya tabianchi

WHO yatoa wito nchi zilinde afya kutokana na mabadiliko ya tabianchi

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetoa wito kwa nchi wanachama zilinde afya ya umma kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, likisema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni suala kuu la karne ya 21. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Kulingana na makadirio ya WHO, mabadiliko ya tabianchi tayari yanasababisha makumi ya maelfu ya vifo kila mwaka, kutokana na mabadiliko kwa mienendo ya magonjwa, majanga ya hali ya hewa kama vile joto kali na mafuriko, na kutokana na uharibifu wa ubora wa hewa, chakula, maji na usafi.

Kwa mantiki hiyo, WHO imesema kongamano lijalo la mabadiliko ya tabianchi (COP-21) jijini Paris, linatoa fursa muhimu kwa ulimwengu siyo tu kuafikia mkataba madhubuti wa kimataifa kuhusu tabianchi, bali pia ya kulinda afya ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

“Kuna faida kubwa za afya ya umma zitokanazo na kufanya maamuzi tunayopaswa kufanya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kupunguza mabadiliko ya tabianchi. Hatua zinazoweza kukabiliana na vichafuzi vya muda mfupi vinaweza kuokoa maisha ya watu milioni 2.4 kila mwaka kufikia 2030 na pia kupunguza ongezeko la joto duniani kwa nusu nyuzi joto. Lakini umuhimu kiafya ni kwamba unaweza kuokoa maisha haya yote kwa kutumia nishati safi.”

Mnamo mwaka 2012, WHO ilikadiria kuwa watu milioni Saba walifariki dunia kutokana na magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa hewa, na hivyo kuufanya kuwa tishio kubwa zaidi la kimazingira kwa afya.