Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa isaidie Somalia kuboresha hali ya haki za binadamu- Simonovic

Jamii ya kimataifa isaidie Somalia kuboresha hali ya haki za binadamu- Simonovic

Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu, Ivan Simonovic, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa iongeze usaidizi wake kwa serikali ya Somalia katika juhudi zake za kuboresha hali ya haki za binadamu.

Bwana Simonovic ametoa wito huo kabla ya kuondoka Mogadishu, kufuatia ziara ya siku tano nchini Somalia, akiongeza kuwa bila usaidizi zaidi kutoka wadau wa kimataifa, ufanisi uliopatikana sasa katika kuendeleza na kulinda haki za binadamu Somalia utakuwa hatarini.

Aidha, amesema kuwa serikali ya Somalia imepiga hatua muhimu katika operesheni dhidi ya Al Shabaab, katika kutekeleza mkakati wa haki za binadamu, kufanyia marekebisho sekta za sheria na usalama, harakati za ujenzi wa taifa na mashauriano kuhusu mwelekeo wa uchaguzi mwaka 2016.

Akikutana na maafisa wa serikali, Simonovic amekaribisha hatua za kuelekea kupitisha sheria ya kuunda tume ya haki za binadamu, na kutoa wito kwa bunge la Somalia kuhakikisha tume hiyo inakuwa huru na kutimiza kanuni za Paris kuhusu viwango wastani vya kimataifa vinavyoongoza kazi ya taasisi za haki za binadamu.