Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya maandalizi dhidi ya El-Nino bado wasiwasi mkubwa : WMO

Licha ya maandalizi dhidi ya El-Nino bado wasiwasi mkubwa : WMO

Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani WMO, Michel Jarraud amesema kwamba athari za El-nino zitaendelea kuongezeka hadi kufikia kiwango cha juu kabisa ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Bwana Jarraud amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini Paris Ufaransa huku akisema kwamba tukio hilo la El-nino la mwaka huu lililosababishwa na kuongoezeka kwa halijoto ya bahari ya Pacifiki, huenda likazidi matukio yaliyotangulia.

(Sauti ya Bwana Jarraud)

« El-nino hiyo ni moja ya El-nino kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Unaweza kukumbuka kwamba El-nino kubwa zaidi iliyopita ilitokea mwaka 1997/1998. Na hii ya mwaka huu inaweza kuwa miongoni mwa El-nino tatu kubwa zaidi. Inaweza hata kuwa kubwa zaidi lakini tutajua katika kipindi cha wiki chache zijazo. »

Aidha amefafanua athari za El-nino, akieleza kwamba ziko za aina mbali mbali ikiwemo kuharibika kwa mwamba tumbawe, kuongezeka kwa idadi ya vimbunga na mafuriko, lakini pia ukame kwenye maeneo mengine ya dunia.

Hata hivyo amesisitiza kwamba kuimarika kwa utabiri wa hali ya hewa na mifumo ya tahadhari na ushirikiano baina ya nchi kumewezesha WMO na wadau wengine kujitayarisha zaidi na kuokoa maisha.

Licha ya mafanikio katika kiwango cha utayarishaji, Bwana Jarraud amesema wasiwasi ni mkubwa kuhusu uhusiano kati ya El Nino na ongezeko la joto duniani.

Amesema ingawa bado utafiti unaendelea kuhusu mada hii, tayari wanasayansi wanatarajia kwamba mwaka huu utashuhudia kiwango cha juu kabisa cha halijoto.