Mashariki ya Kati yaangaziwa Baraza la Usalama, Syria ikibeba ajenda

Mashariki ya Kati yaangaziwa Baraza la Usalama, Syria ikibeba ajenda

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu adhuhuri limekuwa na kikao kuhusu hali ya Mashariki ya Kati huku mzozo wa Syria ukibeba ajenda ya kikao hicho.

Katika hotuba yake Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuhusu usaidizi wa kibinadamu Stephen O’Brien amesema janga la Syria ni kiashiria kwamba Baraza la usalama na wadau wengine muhimu wameshindwa kutumia fursa muhimu kumaliza mzozo huo.

Amesema mzozo unachukua kasi, raia wasiokuwa na hatia wanauawa, waasi wa ISIL na vikosi vya serikali vinazidi kushambulia bila kuchagua, hivyo akasema..

Hali ya sasa Syria haipaswi kuendelea ilivyo. Tumeshuhudia madhara makubwa kwa kutochukua hatua. Hali hii imeondoa imani ya raia kwa jamii ya kimataifa. Wananchi wa Syria wana haki zaidi kuliko mijadala tunayofanya au misaada tunayowapatia: Wanastahili ghasia hiyo isiyo na msingi wowote imalizwe.”

Zainab Hawa Bangura ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono vitani amesema tangu ziara yake kwenye ukanda huo mwezi Mei mwaka huu, anajikita katika kuandaa mikakati ya kuelimisha jamii kuhusu uwepo wa ukatili wa kingono na kwamba ni uhalifu, kwa hiyo…

(Sauti ya Bangura)

“Hatua zetu zisiwei tu za kiusalama na kijeshi. Zinapaswa kujumuisha masuala ya kisheria na utoaji huduma. Uwajibikaji lazima liwe jambo la msingi. Na wakati huo huo, tunapaswa kusaka utashi wa kisiasa hususan kutoka kwa viongozi wa kikanda, kitaifa na eneo husika.”

Wajumbe wa zaraza hilo la usalama kabla ya kuanza vikao vya adhuhuri walisimama kwa dakika moja kukumbuka wahanga wa mashambulio ya Paris, Ufaransa na Beirut Lebanon.