Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano kufanyika London 2016 kuhusu mzozo wa Syria

Kongamano kufanyika London 2016 kuhusu mzozo wa Syria

Viongozi wa Umoja wa Mataifa pamoja na nchi za Uingereza, Ujerumani, Norway na Kuwait, wameeleza kusikitishwa na hatma ya watu wa Syria, na hivyo kutangaza kuwa mnamo Februari mwakani, watafanya kongamano la kimataifa kuhusu mzozo nchini Syria, ambalo litafanyika jijini London, Uingereza.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao wamesema jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuwasaidia watu milioni 13.5 walio hatarini na waliolazimika kuhama ndani ya Syria, na wakimbizi wa Syria milioni 4.2 walioko katika nchi jirani, na kwamba inapaswa kuongeza juhudi hizo.

Kongamano la London litatokana na uzoefu wa makongamano kama hayo yaliyofanyika nchini Kuwait, likilenga kufanya changisho la kujaza pengo la ufadhili, kwani kati ya dola bilioni 8.4 zilizoombwa, fedha zilizokusanywa ni chini ya dola bilioni 3.4.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien, amesema kongamano la London litatoa fursa muhimu ya kuukumbusha ulimwengi kuhusu mateso ya raia wa Syria.